Thursday, 31 December 2015

SALAAM ZA MWAKA MPYA 2016 TOKA JUMUIYA YA MARAFIKI WA KINONDONI





JUMUIYA YA MARAFIKI WA KINONDONI

SALAM ZA MWAKA MPYA 2016

Wanajumuiya,
Ni matumaini ya kila mmoja wetu kwamba mwaka huu 2015 unaisha ukiwa  na changamoto na mafanikio yake. Kwa ujumla, kama Jumuiya mwaka 2015 umekuwa ni mwaka wa mafanikio kwetu tangu tulipoona hitaji la kuwa Jumuiya na tulipoanza utekelezaji wake kwa mbinu na njia mbalimbali. Sote tunakumbuka jitihada tulizofanya katika kuhakikisha Jumuiya yetu inasimama imara na wote tumejitolea kwa hali na mali katika kufanikisha jambo hilo.

Wanajumuiya,
Ni takriban miezi mine (4) tu tangu tuirasimishe Jumuiya yetu kwa kuandaa Katiba na baadaye kufanya uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ambao wanatarajiwa kuhudumia Jumuiya kwa kipindi cha miaka mitati (3) kuanzia mwezi Septemba, 2015 mpaka Septemba, 2018. Hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2015, Jumuiya ina jumla ya wanachama 41. Wanachama hawa wote kwa pamoja wana lengo la kuifanya Jumuiya ya Marafiki wa Kinondoni kuwa ni Jumuiya yenye kuwaunganisha pamoja wakati wote na kuwaletea manufaa. Kimsingi Jumuiy, kama taasisi au mkusnyiko mwingine wowote, ina malengo mbalimbali ambayo ni ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kama ifuatavyo:  -
1.   Malengo ya muda mfupi ((Oktoba 2015 – Machi, 2016)

1.1.      Kusajili jumuiya katika mamlaka za nchi  ili kuifanya iwe rasmi na itambulike kisheria,

1.2.      Kufungua akaunti ya benki,

1.3.      Kupanga ofisi ya Jumuiya,

1.4.      Kuongeza idadi ya wanachama,

1.5.      Kuendelea kukusanya michango na ada mbalimbali toka kwa wanachama ili kukuza mifuko mbalimbali ya Jumuiya.


2.   Malengo ya muda wa kati (Machi 2016 – Machi, 2018)

2.1.      Kubaini fursa mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo kwa Jumuiya,

2.2.      Kuwezesha upatikanaji wa huduma za bima ya afya kwa wanachama wote,

2.3.      Kuanzisha na kuingia ubia wa kibiashara kati ya Jumuiya na Wanajumuiya,

2.4.      Kuanzisha chama cha akiba na mikopo (SACCOS) kwa wanachama na jamii kwa ujumla,

2.5.      Kuongeza idadi ya wanachama,

2.6.      Kuendelea kukusanya michango, ada na tozo mbalimbali toka kwa Wanajumuiya

3.   Malengo ya muda mrefu (2015 na kuendelea)

3.1.      Kuwekeza katika miradi ya ardhi, kilimo na ufugaji,

3.2.      Kuchangia gharama za elimu kwa wanajumuiya wenyewe na watoto/wategemezi wao,

3.3.      Kumiliki eneo (estate) la Jumuiya litakalokuwa na huduma zote za kijamii kama vile, nyumba za makazi za wanajumuiya na familia zao, shule, hospitali, soko, maduka madogo na makubwa, viwanja vya michezo, n.k.

3.4.      Kuingia ubia na kununua hisa kwenye makampuni mbalimbali,

3.5.      Kuanzisha viwanda vidogo vidogo na vikubwa,

3.6.      Kufungua kampuni zitakazojihusisha na biashara mbalimbali,

3.7.      Kuongeza idadi ya wanachama,

3.8.      Kuendelea kukusanya michango, ada na tozo mbalimbali toka kwa Wanajumuiya. 

Wanajumuiya,
Tukiyasoma na kuyatafakari haya malengo yote, tunajifunza kwamba hakuna linaloshindikana iwapo wote tutakuwa na lengo la kutumia vyema fursa vipaji na nafasi tulizonazo katika kuyatimiza yote. Lakini pia, ni ukweli kwamba bila ya nguvu kubwa ya kiuchumi inaweza kutugharimu muda mrefu kufikia angalau robo ya malengo hayo. Yatakapotimia itakuwa ni faida kubwa kwetu sote na vizazi vyetu!

Wanajumuiya,
Mwaka 2016 ni mwaka wetu wa kuthibitisha kuwa sisi ni Jumuiya ya kutolewa mfano kwa masuala yote yanayohusu Jumuiya kama yetu au zinazofanana na Jumuiya yetu. Mtaji mkubwa kabisa tulionao ni huu umoja wetu, kujitoa na kujitolea kwetu na zaidi upendo na ushirikiano wetu. Kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo, hakuna litkalotushinda huko mbele!


Wanajumuiya,
Kwa niaba ya viongozi wote wa Jumuiya ya Marafiki wa Kinondoni, nawatakia heri, baraka, afya njema na mafanikio tele katika mwaka 2016 na miaka mingine yote ijayo.


Yahya Poli,
Mwenyekiti – jumuiya ya Marafiki wa Kinondoni,

Wasiliana nasi: - 
Twitter: @rafikinondoni
Instagram: rafiki_kinondoni


No comments:

Post a Comment